Isack Bilali, BASATA.
“Mnamo mwaka 1996 akiwa bado mtoto mdogo ndipo alipoanza kugundua kuwa ana mapenzi makubwa ya sanaa ya muziki hususani wa asili mara baada ya kumshuhudia baba yake akiwa analichalaza zeze katika matukio tofauti ya shughuli za kiutamaduni, kilimo na sherehe za kijamii ndani ya Kijiji cha Bukene wilayani Nzega, Mkoani Tabora ama kweli ile methali ya Mtoto wa nyoka ni nyoka imeakisi simulizi hii ya Gwiji wa Zeze”
Jilema Ng’wana Shija ni mwanamuziki aliyetimia kutokana na umahiri wake wa kutunga na uandishi wa mashairi yenye kukonga nyoyo za watu, kwa hakika amejaaliwa sana kuwa na uwezo wa kulichalaza zeze kiasi kwamba linamtii na kutoa sauti murua kwa namna anavyoliamuru zinazosindikizwa na mpangilio safi wa sauti zenye kuhamasisha uzalendo na furaha.
Utunzi na uwezo wake wa kuchalaza zeze umemuwezesha kumjengea ujasiri mkubwa wa kutoa tungo mbalimbali zilizokonga nyoyo za mashabiki wa muziki wa asili nchini kupitia nyimbo zake kama vile vijana na ukimwi, chapa ya ng’ombe, Sophia, igembe, selena, mele, niyele na wewe mwananchi ambapo mjumuiko wa nyimbo hizo zinaunda albamu yake aliyoitoa Novemba 4 mwaka 2018.
Anakiri kuwa kwa kipindi hicho wakati anatoa albam ya “Jilema Ng’wana Shija“ hakufanikiwa kupata fedha zaidi ya umaarufu hivyo kumuwia vigumu sana kuendelea kumudu gharama ya kutoa albam nyingine ingawa uwezo bado anao, anaweza kufanya hayo yote kama tu akipata menejimenti nzuri yenye kuthamini maendeleo ya muziki wake.
Mkusanyiko huu wa nyimbo za asili zenye maudhui ya uhamasishaji katika ufanyaji kazi kwa bidi ni mfumo uliomjenga tangu akiwa mdogo na ameurithi kutoka kwa watamngulizi wake hususani Baba yake mzaizi ambaye alikuwa anamshuhudia akitumbuiza katika nyakati za msimu wa kulima na hata kipindi kile cha mavuno ambapo kwa maeneo ya kijijini kwao walitumia mtindo wa kushindana hivyo kuongeza hamasa kwenye uzalishaji.
Ng’wana Shija anaeleza kuwa, mwishoni mwa miaka ya 1980 alitumia muda mwingi kuambatana na Baba yake kila sehemu aliyoenda kutumbuiza kipindi cha msimu wa kilimo ndani ya Mkoa wa Geita, jambo hili lilisababish a kukosa muda wa kujiunga shule na kuhudhuria masomo ya darasani kwa wakati ule akili yake ilimuongoza na kumuaminisha kuwa ujuzi anaoupata ni elimu tosha itakayomsaidia katika Maisha yake hivyo akahamishia jitihada zote kwenye kucheza na zeze.
“Nakumbuka nikiwa mdogo kabisa mwanzoni mwa miaka ya 1980 nilikuwa naambatana sana na Baba yangu kila anapoenda kuimba na kwa kule kijijini hayakuwa matamasha makubwa isipokuwa ni yale ya kushindana na kuhamasisha kufanya kazi kwa bidi hususani wakati wa kulima kwa makundi au mavuno maarufu kwa jina la chapa ya ng’ombe kutokana na kufurahia hali hiyo sikupata nafasi ya kusoma” amesema Jilema.
Kuhama kwa wazazi wake kutoka Mkoa wa Geita kuelekea Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora miaka ya 2000 kulianza kumpa mwanga kwakuwa Baba yake alianza kumuamini na kumuachia asimamie kikundi chao cha muziki wa asili ambapo aliweza kufanya vizuri na kuibuka kidedea hasa kwenye mashindano ya kiutamaduni yaliyoshirikisha makundi mbalimbali ambayo yalihamasisha uzalishaji na uzalendo, umaarufu wake uliongezeka hadi akawa tishio kwa wengine kuogopa kuchuana nae.
Maisha yalianza kubadilika pale alipoamua kwa mara ya kwanza kufunga safari kutoka Mkoani Tabora na kuja jijini Dar es salaam ilikuwa mwaka 2007 ambapo alikuja kwa lengo moja tu kuendeleza muziki wa asili ambapo aliamini kanda ya ziwa ameshajitangaza vya kutosha kilichobaki ni kumfikia kila mtanzania na sehemu peke ya kufanikisha mkakati wake ni Dar es salaam.
Alipowasili jijini hakuapata changamoto sana kwakuwa alikuta wenyeji alioweza kushirikiana nao wakamuonesha njia na mbinu za upambanaji lakini kikwazo kikubwa kilikuwa ni udhaifu wake wa kutokujua kusoma wala kuandika, Maisha ya mjini yanaweza kuwa rahisi endapo kipaji kitaambatana na kujua kusoma na kuandika kwakuwa vitu havifanyiki kiholela hata kazi inapatikana kwa kusainiana mikataba hivyo ikamlazimu kuanza kujifunza kusoma na kuandika jambo ambalo halikumchukua muda mrefu.
Mara nyingi aliweza kupata kazi za kupiga katika maeneo mbalimbali ya starehe zikiwemo hoteli kubwa na kwenye lumbi za burudani hizo kazi zilimsaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kuendesha Maisha yake ya hapa mjini hasa kupata mahitaji ya msingi, aliweza kufanya kazi zake kwa miaka 6 akarejea tena kwao Tabora kabla ya kurudi tena Dar es salaam mwaka mmoja baadae yaani 2014.
Jilema anaweka wazi kuwa mara baada ya kurejea mjini alianza kuona nyota imeanza kumuwakia kwani kazi zake zilianza kupata kibali cha mialiko ya kwenda kutumbuiza katika baadhi ya nchi za Afrika na Ulaya kwenye matamasha yenye hadhi ya kimataifa kutokana na mjumuiko wa washiriki wake kutoka maeneo mbalimbali Duniani ikiwemo Kenya 2016, Zambia 2017, Uturuki 2016, Denmark 2016, Ujerumani 2017, Norway 2019 zilimuwezesha kutanua wigo wa kufahamika kwa wadau mbalimbali ingawa hakuweza kuendelea kufanya nao kazi kutokana na kukosa menejimenti ya kumsimamia.
Pamoja na kipindi kirefu kuwa kimya huku akiendesha shughuli zake kupitia kutumbuiza katika Hoteli mbalimbali lakini sasa ameona umefika muda wa yeye kusimama tena kwakuwa serikali imeshaanza kutilia mkazo sekta ya sanaa hivyo ana matumaini makubwa kuwa kila jambo litaendelea kufanyika kiiutaalama ili kuboresha mnyororo wa thamani utakaomnufaisha kuanzia mzalishaji hadi msikilizaji wa maudhui ya kazi za sanaa.
Kutokana na hilo, ameiomba serikali kutilia mkazo mfumo wa elimu ya sanaa uwekwe katika somo kuanzia ngazi ya msingi ili kuwavuta wenye vipaji kama yeye wasikwepe kupata ujuzi huo kwa wakati, hapa, anaamini kwamba hata yeye wakati akiwa mdogo angeweza kuhudhuria masomo yake vizuri tu iwapo kungekuwa na elimu ya sanaa inayototolewa kikamilifu.
Sanaa sasa hivi ajira hivyo tunatakiwa kujivunia utamaduni wetu ili uwe kielelezo kwa watu wengine pale endapo sanaa yetu itafanikiwa kuvuka mipaka, ingawa katika hili kuna kasumba inayotawala hata miongoni mwa wasanii wenyewe kuwa matumizi ya ala za asili katika sanaa ni “ushamba” hii inatokana na usasa na kutothamini cha kwako jambo ambalo analipinga vikali Jilema Ng’wana Shija huku akimpa Kongole mwanamuziki mahiri Marioo ambaye alidiriki kumshirikisha kuweka “kionjo” katika wimbo wake wa “Hakuna Matata” ambao unaendelea kukimbiza sokoni.
Kwa sasa yupo katika hatua ya kutafuta wadau ambao wataweza kumsimamia kazi zake kulingana na mfumo wa soko la sasa kwakuwa bado ana utajiri mkubwa tungo zenye kusisimua, pia anakaribisha wasanii mbalimbali kushirikiana kwenye kazi kwakuwa utamduni ni kielelezo cha uzalendo, kujirasimisha ni msingi wa kuzikaribia fursa za sanaa zinazochagizwa na sera nzuri serikalini.