14 Juni, 2024
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Dkt. Damas Ndumbaru leo tarehe 14 Juni, 2024 amehimiza wasanii kujiraismisha ili kurahisisha mipango ya serikali ya kuwatafutia fursa mbalimbali kwakuwa sanaa ni ajira inayoingiza kipato halali.
Ameyasema hayo wakati anazungumza na watu mashuhuri wakati wa hafla maalum ya kujadiliana mchango wa celebrities katika kujenga afya ya bora ya akili na maadili katika kazi za sanaa kwenye ukumbi wa Serena jijini Dar es salaam.
Mhe. Waziri ameongeza kuwa, serikali ya awamu ya sita imekuwa Mstari wa mbele kupambania maendeleo ya wasanii ndo mana imefufua mfuko wa utamaduni ambao unawawezesha wasanii ambapo hadi sasa umefanikiwa kutoa kiasi cha fedha shilingi Bilioni 4.2 kwenda kwa wasanii mbalimbali nchini.
Juu ya hapo, tunapaswa kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mahaba anayoendelea kuyaonesha kwenye tasnia ya Sanaa kwani kupitia hotuba yake wakati wa tukio la uzinduzi wa albamu ya Msanii Harmonize ametamka rasmi kuambatana na wasanii katika ziara zake ili kuwafungulia fursa za soko la Kimataifa.
Hayo yote yanawezekana kufanyika kwa usahihi na ufanisi kulingana na utayari wa kujiweka katika mfumo rasmi hivyo amewasihi wasanii wote kujirasimisha kwa wakati ili muda utakapofika usirukwe kwa sababu za uzembe.
Mwisho, amewapongeza wasanii waliohudhuria mafunzo pamoja na watoa mada katika mkutano maalum ambapo makala zote zilizofundishwa kuhusu afya bora ya akili, mikataba katika kazi za sanaa, uzingatiaji wa maadili katika kazi za sanaa na usalama na uzalendo wa nchi yanaakisi maendeleo ya sekta ya sanaa nchini.